WAHUKUMIWA MIAKA 20 JELA KWA KUWAUA ALBINO SUMBAWANGA. - KABONGE BLOG.

Blog hii ni kwaajili ya masuala/taarifa za kidini na matukio yanayotokea kila siku.

Breaking

Friday, September 1, 2017

WAHUKUMIWA MIAKA 20 JELA KWA KUWAUA ALBINO SUMBAWANGA.

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga imewahukumu miaka 20 jela kila mmoja watu 9 baada ya kuwatia hatiani kwa kushiriki kuwakata mikono walemavu wa ngozi wawili na kusababisha ulemavu wa kudumu.

Hukumu iliyosomwa kwa takribani masaa mawili na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga Jaji Dr. Adam Mambi katika mahakama kuu Kanda ya Sumbawanga juu ya mashauri mawili yanayohusu ukatili dhidi ya wenye ulemavu wa ngozi, Albino.

Katika shauri la Jinai No. 1 ya mwaka 2015 watuhumiwa sita wametiwa hatiani kati ya kumi kwa kutenda makosa mawili, kula njama ya kutaka kuua kinyume cha sheria ya kanuni ya adhabu kifungu cha 215 sura ya 16, kufanya jaribio la kutaka kuua, katika kosa la kwanza watuhumiwa wamehukumiwa kifungo cha miaka 14 jela na kosa la pili wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, adhabu zote zikienda pamoja.

Waliohukumiwa katika shauri hili kutumikia miaka 20 jela ni; Weda Mashilingi, Ignas Sungura, James Paschal, Nickson Ngalamika, Ibrahim Tela na Faraja Jairos.

Katika shauri la jinai No. 46 ya mwaka 2015, watuhumiwa watatu wamepatikana na hatia, wawili kati yao wametenda makosa matatu ya kula njama ya kuua, kufanya jaribio la kuuwa na kusababisha ulemavu wa kudumu kwa mwenye ulemavu wa ngozi, Maria Chambanenje katika tukio lililotokea Februari 2013 katika kitongoji cha Mkole kata ya Miangalua wilaya ya Sumbawanga.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Jaji Dr. Adam Mambi amewahukumu watuhumiwa watatu kati ya wanne waliokuwa wanashitakiwa katika makosa hayo na kumuacha huru mtuhumiwa mmoja baada ya kusikiliza pande zote na kuridhika kuwa watuhumiwa wawili walihusika kutenda makosa yote matatu na mmoja alitenda kosa moja la kula njama ya kutaka kuua.

Jaji Dr. Mambi amemhukumu Togwa Cosmas kutumikia jela miaka 14 kwa kutenda kosa moja na wenzake wawili Linus Silukala na Maiko Kazanda wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia katika makosa yote matatu.

Nje ya mahakama nimezungumza na waliohudhuria hukumu hizo zikisomwa mahakamani hapa akiwemo mkuu wa mkoa wa Rukwa ambaye ameipongeza mahakama kwa kutenda haki kwa watuhumiwa.

No comments:

Post a Comment