MASOMO YA DOMINIKA YA 26 YA MWAKA A WA KANISA. - KABONGE BLOG.

Blog hii ni kwaajili ya masuala/taarifa za kidini na matukio yanayotokea kila siku.

Breaking

Saturday, September 30, 2017

MASOMO YA DOMINIKA YA 26 YA MWAKA A WA KANISA.

DOMINIKA YA ISHIRINI NA SITA YA  MWAKA  A.
MASOMO.
Eze.18 :25-28.
Flp.2:1-11.
Injili Mt 21: 28-32.

WAZO KUU:MANENO  MAZURI  HAYACHUKUI  NAFASI  YA MATENDO MEMA.
UTANGULIZI.
Ndugu zangu,leo ni Dominika ya Ishirini na sita ya mwaka A wa kanisa.Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuongoza juma lililopita.Tumefika tena nyumbani mwake kusudi tumshukuru,tumsifu,na tumuombe kwaajili yetu na wengine ili atujailie neema zake kwa juma tulililoanza.Masomo yetu yanatutafakarisha juu ya kupokea neno la Mungu na kulitekeleza kusudi tupate kuokoka.Utekelezaji huo unahitaji unyenyekevu wa mtu binafsi na umoja na wengine.Nimechagua wazo hili Maneno mazuri hayachukui nafasi ya matendo mema,lisindikize tafakari ya masomo yetu leo.

UFAFANUZI.
Ndugu zangu,katika somo la kwanza mwenyezi Mungu kwa kinywa cha nabii Ezekieli anasema kuwa Mungu mwenye huruma atamsamehe dhambi zake na kumuhuisha muovu anayetubu.Lakini kwa upande wa pili atamuadhibu na kumuangamiza mtu aliyekuwa  mwenye haki na mwema ambaye amepotoka na kugeukia njia ya  uovu.Mungu anatazama hali ya mtu ya sasa bila kuhesabu mambo yake ya kale.Hivyo kwa haki ya Mungu kwa mkosefu anayetubu inamuokoa si tu  kwa  dhambi ya mababu Adamu na Eva bali pia kwa dhambi zake hata za kale.Mwenye haki anayeacha matendo mema na kugeukia uovu anaadhibiwa katika uovu wake wa sasa.Nabii anaeleza uwezekano wa msamaha kwa mtu anayetubu maovu yake yote hata ya kale,lakini pia nabii anaeleza hatari ya kupoteza mazuri yote aliyofanya mtu siku za nyuma kwasababu ya kuugeukia uovu.

Katika Injili tumesikia mfano wa Yesu juu ya wana wawili wanaomkosea baba yao.Mtoto wa kwanza anaambiwa na baba yake aende akafanye kazi katika shamba  la mizabibu na anakubali kwa  “ndiyo” lakini kumbe hakuenda.Huyu amemkosea baba yake kwa kutotekeleza alililoambiwa hata kama aliitikia vizuri.Amemdanganya Baba yake.Mtoto wa pili anaambiwa nae vilevile aende kwenye shamba la mizabibu akafanye kazi.Huyu anajibu “sitaki”.Kumbe baadae anajihoji,anaenda kwa babae anatubu na kwenda shambani kufanya kazi.Huyu nae amemkosea baba yake kwa kumjibu vibaya hata kama baadae alienda kufanya mapenzi ya baba yake.Kati ya hawa wana wawili wakosefu huyu wa pili anaonekana kuwa ni nafuu kuliko yule wa kwanza.Wote wawili ni wakosefu kwasababu ilitakiwa wanapoambiwa na baba yao wakubali kwa ndiyo na waende wakafanye kazi.Yote mawili! Yesu anafundisha umhimu wa matendo na si maneno matupu.Yesu anaeleza kuwa makahaba na watoza ushuru wanaotubu watafika Mbinguni.Makahaba na watoza ushuru ni wawakilishi tu wa wale wote wanaokosa uaminifu kwa mapenzi ya Mungu na wanaotenda uovu ambao wanaitwa wadhambi.Hawa kwahiyo ni Ishara ya dhambi.

Katika somo la pili Mtume Paulo anasema kuwa Yesu kristo ametuonesha mfano wa kushika unyenyekevu kwa tendo lake la kuchukua mwili wa kibinadamu,kuteswa na kufa msalabani.Unyenyekevu huo wa Yesu haukuwa kwa manufaa yake bali kwa manufaa ya mwanadamu.Kwa kuiga mfano wake mwanadamu ajibidishe kujivika unyenyekevu na  awafikirie na kuwajali wengine,ili kuwavutia watu kwa Mungu na kumpeleka Mungu kwa watu.Kinachomsaidia kufaulu katika unyenyekevu ni muungano na wengine katika upendo.Kumbe majivuno yaliyo kinyume na unyenyekevu huleta utengano kwasababu,mwenye majivuno huongozwa na tamaa binafsi na kujifikiria binafsi.Paulo anasisitiza juu ya umoja kwa vile ubatizo unatufanya tuwe ndani ya Kristo na kumshiriki Roho Mtakatifu.Nguvu ya upendo wa kikristo inatuungamisha.Hisia za kibidamu tu bila nguvu hiyo  huuondoa umoja na bila umoja na wengine hakuna furaha.

MAISHANI.
Ndugu zangu,Kutekeleza mapenzi ya Mungu kunamfanya mtu kuwa mwenye haki.Yesu anasema “Si kila asemaye Bwana Bwana  ataingia katika ufalme wa Mbinguni,bali yule anayetimiza mapenzi ya Baba yangu aliye Mbinguni”(Mt 7:21).Toba kwa wanaotubu inawaondolea si dhambi yao tu bali pia adhabu waliyostahili kwa dhambi waliyotenda.Hivyo ni kweli kwamba wenye dhambi ni lazima watubu kwanza ndipo wapate kuingia Mbinguni.Yesu anaonesha kuwa wadhambi hao ni rahisi kutubu na kubadili misimamo yao  kuliko wale wanaojiona ni watu wema.Hivyo wakosefu wanatiwa moyo na kuhakikishiwa kuwa watakubalika na Mungu ili mradi tu wanatubu.Wale wanaojiona ni watu wena wanaalikwa kujichunguza zaidi na kupima wema wao unafika mpaka wapi.Katika kanisa tunajikuta wote tu wakosefu.Tunaweza kuwa ni wakosefu kama mtoto wa kwanza au kama yule wa pili.Lakini ilipasa tuwe watoto wa wema.Ni hivi:

Wapo katika kanisa wanaokiri imani ya kanisa kwa kinywa bila utekelezaji kama yule mtoto wa kwanza.Hawa wanaweza kuwa kwa nje ni watu wa “ndiyo Baba” ,wa sala na nyimbo nyingi,wa makongamano na mikesha lakini kwa siri ni hao hao wanaofanya mauaji,wanavuruga ndoa,wanaobomoa na kuiba,wanaokosa uaminifu katika viapo vyao.Tena wanaweza kuwa ni watu waliobatizwa na kupata sakrementi zingine za kanisa sasa wameacha kuendelea katika safari ya matendo ya maisha ya imani yao.Hawa wanakumbushwa kuwa maneno matupu hayawezi kuchukua nafasi ya matendo mema.
Wapo tena wengine ambao hawakiri imani ya Kanisa na wala hawana mpango na kanisa lakini wanaishi vizuri na wengine kuliko hata wale wanaojiona ni washika imani.Hawa ni kama yule mtoto wa pili.Hawa nao pia wanakosea kwa kutomsikilia Mungu aliyejivunua kwao.Ingawa wanaweza kuishi vizuri na wengine bado hawamkiri Mungu na hivyo hawawezi kumfahamu vizuri na kutekeleza barabara mapenzi yake.Hawa hawakiri ufunuo wa Mungu katika Yesu Kriso na hivyo wanajiona kuwa wamejikamilsha na hawamhitaji Mungu.

HITIMISHO.

Ndugu zangu,masomo yetu yanatutaka tuwe watu wema.Mtu mwema mbele ya Mungu ni yule anayekiri na kutekeleza mapenzi ya Mungu.Tusiwe kama yule mtoto wa kwanza na wala yule wa pili.Inafaa tuwe watoto wanaosema “ndiyo” na wanatekeleza mapenzi ya Baba.Kama angekuwepo mtoto wa namna hii katika mfano wa Yesu angekuwa labda mtoto wa tatu.Tusikate tamaa katika mapungufu yetu.Lakini tujue kuwa maneno matupu hata kama ni matamu namna gani hayawezi kuchukua nafasi ya matendo mema.Tena tusisahau kuwa ni rahisi kuharibu jambo jema kwa namna au mtindo anaotumia mtendaji.Njia ya Kikristo ni kutenda jambo jema kwa namna nzuri.

Tumsifu Yesu Kristo!
Na Padre Augustino Kamnyuka.
Parokia ya Kristo Mfalme Bologna-Italia.
Tarehe 01.10.2017.

No comments:

Post a Comment