KARIBUNI KWA TAFAKARI YA MASOMO YA DOM YA 32 MWAKA C WA KANISA. - KABONGE BLOG.

Blog hii ni kwaajili ya masuala/taarifa za kidini na matukio yanayotokea kila siku.

Breaking

Saturday, November 5, 2016

KARIBUNI KWA TAFAKARI YA MASOMO YA DOM YA 32 MWAKA C WA KANISA.

DOMINIKA YA 32 YA MWAKA C
MASOMO:

SOMO LA KWANZA
2Mak 7:1 – 12, 9 – 14.

SOMO LA PILI
2Thes 2: 16 – 3:1 – 5.

INJILI
Lk 20:27 – 38.

WAZO KUU:  TUISHI NA KUMALIZA VIZURI MAISHA YETU YA DUNIANI.

UTANGULIZI.
Ndugu zangu, leo ni Dominika ya 32 ya Mwaka C wa Kanisa. Tupo ndani ya Mwezi Novemba, mwezi ambao Kanisa letu linatuhimiza kutafakari maisha yetu ya baada ya kumaliza maisha ya hapa duniani. Kanisa limeweka mbele yetu mwezi huu kuwashangilia na kuwaomba watakatifu wa mbinguni watuombee na papo hapo kuwaombea ndugu zetu marehemu walio Toharani. Katika Dominika ya leo, masomo yetu yakituhimiza kuishi na  kumaliza vizuri maisha yetu ya hapa duniani. Maana, mwisho wa maisha yetu ya hapa duniani unauhusiano na maisha mapya. Tumalize vizuri maisha yetu ya hapa duniani, ili tupkaishi kuzuri.
UFAFANUZI.
Ndugu zangu, katika somo la kwanza toka kitabu cha pili cha wamakabayo, tumesikia kile walichojibu vijana wanne kwa Mfalme walipokuwa kufani sababu ya imani yao. Ndugu hao waliokuwa saba pamoja na mama yao, walilazimishwa kula nyama marufuku ya  nguruwe iliyo kinyume na imani yao ya dini yao ya kiyahudi. Ndugu wote saba pamoja na mama yao walikataa amri hiyo wakaona ni bora kufa kuliko kuvunja imani yao. Somo la leo limetuletea majibu ya wale watoto wanne wa mwanzo kati ya wale saba pamoja na mama yao. Majibu yao ni maungamo ya kijasiri ya imani katika ufufuko wa wafu. Ndugu hao wana ujasiri wa kutolea uhai wao kwasababu wana uhakika kwamba Mungu atawajalia uhai mwingine. Maana, “Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo” (Ebr 11:1).

Katika Injili tumesikia Masadukayo, wakimuuliza Yesu swali la kumtega juu ya maisha baada ya maisha ya hapa duniani. Wanamtega kwa kubuni kisa cha mwanamke aliyeolewa kwa ndugu saba kwa kufuata sheria ya ndoa ya kurithi mke, (Rejea Mwa 38:8, Kumb 25:5 – 10) iliyodai kuwa ndugu yaani kaka analazimika kumrithi mke wa marehemu kaka yake kama kaka aliyekufa hakuacha mtoto wa kiume, ili amzalie kaka yake aliye kufa mtoto wa kiume. Masadukayo watu wasio amini maisha baada ya kifo, wala uwepo wa Roho na malaika, na wanaopokea mafundisho ya vitabu vitano vya Musa tu, wanamhoji Yesu kuwa kama kuna ufufuko wa wafu, mwanamke aliyeolewa kwa ndugu saba wakafa mmoja baada ya mwingine na mwisho akafa yule mwanamke naye, katika ufufuko atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa kwa wote saba. Yesu analipangua swali hilo katika vipengele viwili. Kwanza anawaeleza ukweli kuhusu ufufuko. Anatumia vitabu vile vile wanavyoamini masadukayo kuwa Musa anamuita Mungu ni Mungu wa  Abrahamu, wa Isaka na Yakobo, mababu ambao walisha kufa zamani.
Katika imani ya kiyahudi kumuita Mungu ni Mungu wa fulani lazima fulani huyo awe hai. Kwa kusema hivyo Musa alionesha kuwa Abrahamu, Isaka na Yakobo ni hai. Yesu anawaonesha masadukayo ujinga wao ya kuwa hawakujua vema maandiko matakatifu ya kuwa kuna maisha baada ya kifo.Pili, Yesu analipangua swali lao kwa kuonesha hali ya watu walio katika utukufu. Kwamba maisha ya kuoa au kuolewa yanakoma hapa hapa duniani. Hali ya miili ya watu wafufuliwa haitatawaliwa na hisia za sasa.Kwahiyo maisha ya ndoa hayatakuwapo tena. Yesu anawaonesha masadukayo ujinga wao wa kutojua maisha yatakavyokuwa baada ya ufufuko.
Mtume Paulo katika waraka wake wa pili kwa Wathesalonike, somo tulilosikia leo, anasali kwaajili ya kutiwa moyo kwa Watheselonike ili waache hali yao ya wasiwasi, ili waimarike, waendelee kuishi maisha mazuri ya kikristo.
MAISHANI.
Ndugu zangu, mwanadamu ana uwezo wa kuamua mahali pake pa Roho yake,mahali  kuishi baaada ya kumaliza maisha yake ya hapa duniani. Mtindo wa maisha anayoishi sasa na namna atakavyo maliza maisha yake ya  hapa duniani, ndiyo unaoamua mahali pa atakapo kuwapo. Kanisa linatufundisha kuwa,ili tupate kufika Mbinguni haitoshi tu kubatizwa na kusadiki Neno la Mungu,yatupasa bado kuepukana na dhambi na kushika sheria za kikristo.Ndugu zangu,mimi nafikiri kuwa ni busara kuandaa maisha mapya ya baadae.Tufanyeje kuyaandaa maisha yetu ya baadae?

Mosi,Tuifahamu vizuri imani yetu na kuiishi.Tushike vema imani yetu juu ya Mungu Baba,imani juu ya Mungu Mwana,imani juu ya Mungu Roho Mtakatifu na Imani juu ya Kanisa letu,moja Takatifu,katoliki na la mitume.Tushike vema amri za Mungu na za kanisa lake,na tupokee Sakramenti za kanisa lake na tusali.Ufahamu mzuri wa imani yetu ni msaada wa kutusaidia ili kuishika vema.Kama Masadukayo wangefahamu vizuri  Maandiko Matakatifu,wasingeingia kwenye fedheha ya bure ya kutojua ukweli juu ya ufufuko na hali ya watu waliofufuliwa.Kama tunavyofanya bidii kujifunza katika shule mbalimbali,kama tunavyofanya bidii kupeleka watoto kwenye shule nzuri ili wapate ili nzuri,au kama tunavyofanya bidii kufundisha wanafunzi wetu waelewe vizuri masomo yao,ni lazima pia kufanya bidii ya kusoma,kusomesha na kufundisha vizuri zaidi imani yetu.Elimu dunia ni mhimu sana kwa maisha yetu.Lakini elimu hiyo itusaidie kuifahamu na kuiishi imani yetu ambayo yatufaa si hapa duniani tu bali pia kutuwezesha kufikia maisha  mapya ya heri ya milele Mbinguni.

Pili,Tusiwe watoto katika imani.Tusivutwe huko na huko na kila aina ya upepo na mafundisho kinyume na imani yetu. Kanisa katoliki linaamini katika uhuru wa kuabudu na linaheshimu watu wa dini na madhehebu yote. GS.26.Waamini wakatoliki tusishawishike kutenda jambo lolote kinyume na maelekezo ya upendo wa kiinjili.Waamini tusitumie muda wetu kuhubiri juu ya imani zisizotuhusu.Waamini wakatoliki tujikite katika kuijua na kuiishi imani yetu kwa kina.Waamini tuwe macho tukidumu katika sala na tuwe wapole kama hua na  wenye busara kama nyoka (Mt. 10:16).

Tatu,Ushuhuda wa imani si lazima kumwaga damu,yaani kufa kishahidi. Ni kumshuhudia Kristo katika mazingira yetu.Kwanza katika Mazingira ya Familia,Familia ni kanisa la kwanza la nyumbani na la msingi la malezi mhimu ya imani na kiutu.Familia ziipeleke nyumbani imani ziliyoipokea na kuiishi na kuijengea mazingira ya kukua.Pili Katika mazingira ya Kazini na katika jumuiya.Mwaliko wa kuishuhudia imani, unaanzia kanisani na katika familia na unatekelezwa popote tunapokwenda.Mkristo Mkatoliki  asifikiri kuwa imani ni tendo la kisiri, bali anapaswa kuipeleka imani katika jamii kama tendo la ushuhuda wa kikristo.Huku ndiko kuwa chimvi na nuru ya ulimwengu kama walivyofanya Vijana wanne tuliosikia leo katika somo la kwanza. Tusikubali kupoteza imani yetu hata katika mazingira magumu. Kor :1:23
Nne Kuna Maisha baada ya kifo.Kadiri ya Mafundisho ya Kanisa Katoliki, binadamu ambaye ni Mwili na Roho; anapoteza uhai wake pale mwili wake unapotengana na roho yake na hapo tunasema binadamu huyo amefariki. Kumbe mara baada ya mtengano wa roho na mwili yaani mara baada ya kifo, hufuata hukumu yaani kutoa zawadi au adhabu kwa roho yake kadiri ya matendo ya mtu huyo. Kama matendo ya mtu yalikuwa ni mazuri anapewa zawadi, wakati kama matendo yake yalikuwa ni mabaya anapewa adhabu. Mtoaji wa hukumu hiyo ni Mungu mwenyewe. Hapo Mungu huihukumu roho ya binadamu kwenda moja kati ya hali tatu yaani: mbinguni, toharani au motoni. Kama mwanadamu aliishi vyema na kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu, akafa katika hali ya neema ya utakaso,  huenda moja kwa moja mbinguni; kama aliishi  vema, lakini akafa katika hali ya  mapungufu machache, roho yake  huhitaji kutakaswa kabla ya kufika Mbinguni. Na hivyo roho yake huenda toharani. Kumbe kama binadamu huyo aliishi vibaya na hakutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu tena akafa akiwa amemkataa kabisa Mungu, roho ya binadamu huyo huhukumiwa kwenda motoni au Jehanamu ambako moto wake na mateso yake ni ya milele. Ikumbukwe kuwa mbinguni, toharani na motoni; ni hali na sio mahali. Tuamue vizuri sasa mahali pa maisha yetu baada ya maisha ya sasa ya hapa Duniani.
HITIMISHO.
Ndugu zangu, Roho ya mwanadamu aliyejaliwa uhuru, inaweza kuchagua mahali pake baada ya maisha ya sasa. Mwanadamu anaweza kutumia muda na vitu kuamua mahali pa roho yake,na hukumu yake. Ukweli kwamba wanadamu huanguka kiroho ni kweli pia wanao uwezo wa kuinuka au kuamua kubaki katika anguko lao.

Tumsifu Yesu Kristo!
Na Padre Augustino Kamnyuka.
Parokia ya Ulete
06.11.2016

No comments:

Post a Comment