DOMINIKA YA ISHIRINI NA SABA YA MWAKA A.
MASOMO.
Isa.5 :1-7.
Flp.4:6-9.
Injili Mt 21: 33-43.
WAZO KUU. SASA NI WAKATI WA KUZAA MATUNDA MEMA YA IMANI.
UTANGULIZI.
Ndugu zangu,leo ni Dominika ya Ishirini na Saba ya Mwaka A wa Kanisa.Dominika iliyopita tulitafakari juu ya kutekeleza neno la Mungu si kwa maneno tu bali pia kwa matendo.Leo Neno la Mungu linatuhimiza kuwa utekelezaji huo wa Neno la Mungu uzae matunda mema.Tumuombe Bwana atujalie neema zake ili katika wajibu zetu tulizokabidhiwa tuzae matunda mema ya matendo mema.Tutafakari masomo yetu ya Dominika ya leo tukiongozwa na wazo hili, Sasa ni wakati wa kuzaa matunda mema ya imani.
UFAFANUZI.
Ndugu zangu,katika maandiko matakatifu manabii na hata Yesu mwenyewe walitumia mara nyingi mifano ili kufikisha ujumbe kwa walengwa.Leo katika somo la kwanza tumesikia nabii Isaya akitumia mfano wa shamba la mizabibu kwa mtindo wa shairi.Nabii anasema mtu mmoja aliandaa shamba lake la mizabibu,kilimani mahali pa rutuba kubwa,akaweka handaki kulizunguka ili kulikinga na waharibifu,akatoa mawe yaliyokuwemo,akajenga mnara kwaajili ya ulinzi,akachimba shimo la shinikizo ndani yake akapanda zabibu akitegemea kupata mavuno bora na manono toka shambani mwake.Kumbe mizabibu ya shamba lile ikazaa zabibu chachu,zabibu mwitu.Mwenye shamba anahoji kilikosekana nini mpaka ikazaa zabibu mwitu? Jibu lake ni hakuna kilichokosekana kwa upande wa mwenye shamba, na hivyo shamba lile linastahili kubomolewa tu maana halina faida,halifai kitu.Linastahili adhabu ya kuondolewa.Nabii anatumia mfano huu kueleza kuwa mwenye shamba la mizabibu ni Mungu,mizabibu yenye dhamani ni waisraeli,ardhi nzuri ni nchi ya Israeli,mawe yaliyoondolewa ni mataifa mengine yaliyoondolewa ili waingie waisareli toka Misri.Matunda mazuri yaliyotarajiwa ni matendo mema,uaminifu kwa Agano,haki kwa jamii,na upendo kwa masikini,yatima na wajane.Kumbe Taifa hilo pamoja na matunzo ya Bwana halikutoa matunda mema ya matunzo hayo bora.Hivyo kama lile shamba la mizabibu wanastahili adhabu.
Katika Injili Yesu anawambia wakuu wa makuhani na wazee mfano unaofanana na ule wa nabii Isaya.Mfano wa wakulima wabaya katika shamba la mizabibu.Yesu anasema kulikuwa na mtu mwenye shamba lake zuri alilolianda na kutulitunza vizuri kwa kulifanyia mahitaji yote mhimu.Kisha akalikodisha kwa wakulima kwa mapatano kuwa atakuja kuchukua matunda yake wakati wa mavuno.Kisha yeye akasafiri.Wakati wa mavuno aliwatuma watumishi wake waende kwa wakulima wale wakapokee matunda ya shamba lake.Wakulima waliwatenda vibaya wale watumishi,akatuma wengine mara ya pili nao wakawatenda vilele na mwishoni akamtuma mwanae akitumaini kuwa watamstahi.Kumbe huyu wakamtoa nje ya wigo na kumuua.Yesu anawauliza wakuu wa makuhani na wazee huyu mwenye shamba atawafanyaje hawa wakulima.Jibu lao ni atawaangamiza vibaya na shamba atawapangisha wakulima wengine.Yesu anaeleza mfano huu akimaanisha kuwa Shamba la mizabibu ni Taifa la Israeli,Mwenye shamba ni Mungu,Wakulima ni viongozi wa Taifa la Israeli,Watumishi ni manabii waliotumwa na Mungu,mwana wa mwenye shamba ni Yesu Kristo na wakulima wapya ni viongozi wapya wayahudi na wasio wayahudi wa taifa jipya yaani kanisa.
Katika somo la pili tumesikia mtume Paulo akiwaambia wenzetu wafilipi na anatuambia pia sisi kuwa waondoe tofauti zao ili Injili isonge mbele.Kwa njia ya sala wamtolee Mungu shida na mahangaiko yao yote.Wasali kwaajili yao na wengine wakimshukuru Mungu.Wajifunze yale waliyoyaona na kusikia toka kwake na wayatendee kazi ili kujipatia amani.
MAISHANI.
Ndugu zangu,ukristo ni Maisha.Baada ya muda mrefu tangu tulipopokea imani ya Kikristo na baada ya kupokea neema ya upendo wa Mungu katika maisha yetu,tunapaswa sasa kuzaa matunda ya upendo huo.Mungu wetu anatutaka tuzae matunda ya matendo mema,ya haki,na uaminifu katika imani tuliyopokea. Mimi leo napenda tutafakari kuwa.
Kwanza tutimize vema wajibu zetu. Mungu ametupatia wajibu wa kuwajibika.Ametupatia majukumu kila mmoja wetu ya kufanya na anatutaka tutende mema.Ingawa mara nyingi tunakosea tena na tena,Mungu wetu anatuvumilia na kuwatuma wajumbe wake tena na tena ili kutufundisha kutuonya na kututahadharisha juu ya yatakayotupata baadae.Kama wakulima wa shamba lake anataka kwetu matunda ya shamba la wajibu zetu.Tusifikiri kuwa atatudai yanayozidi uwezo wetu,la hasha! Yale tuliyopokea kwake na muda tuishio hapa duniani ni wa kutenda matendo yazaayo matunda mema.Kila mmoja wetu katika karama na fadhila alizojaliwa atapaswa kutoa matunda mema.Mungu atatoa hukumu ya haki na tutawajibika kwa wajibu zetu.Tutimize vema wajibu zetu.
Pili, tutumie vizuri uhuru wetu.Mungu ametupatia uhuru katika kuwajibika,ametupatia uhuru katika kutekeleza wajibu zetu.Huu pia ni upendo wake mkubwa kwetu wa kutaka tutumie utashi wetu kutenda lililo jema.Ametukabidhi kazi ya kufanya bila nyapara wa kutusimamia.Matumizi mabaya ya uhuru huo ndiyo sababu ya kutenda dhambi.Kwa kusudi tunaweza kuvunja maagano imani yetu na kutenda yasiyo.Lakini tusisahau kuwa pamoja na upendeleo huo,na uhuru aliotujalia tutapaswa kujibia juu ya matendo yetu.Tutapaswa kumpa matunda mema ya shamba lake.Tutumie vizuri uhuru wetu.
Tatu upendo wa Mungu unazidi hata uhuru wetu.Tunapotafakari wazo hili kila mmoja arudi nyuma na kuona maisha yake.Mara ngapi ametumia uhuru wake vibaya akachagua kumtupa nje ya wigo Bwana wake Yesu,mara ngapi ametupa nje makubaliano ya agano lake la viapo vya ubatizo,mara ngapi ametupa nje viapo vyake vya maisha ya ndoa,utawa au upadre.Mara ngapi ameshindwa kutimiza matendo ya haki na upendo kwa wahitaji kama inavyofundisha Injili.
Mungu wetu pamoja na matumizi mabaya ya uhuru wetu amemtoa mwanae pekee Yesu Kristo atoe sadaka ya kifo cha aibu msalabani kwaajili ya wokovu wetu.Kifo chake ni sadaka ya wokovu kwa wanadamu.Kristo anapotolea mfano wa wakulima wabaya alijua kuwa ni yeye mwenyewe atakaye uawa na kutupwa nje kwa ubaya wa dhambi zetu.Tuujibu upendo wake kwa kupenda mema na kuyatenda.
HITIMISHO.
Ndugu zangu,Mtume Paulo ametuhimiza tusali ili kujipatia neema ya kutusaidia kutimiza vema wajibu zetu.Anayesali kwa tumaini kamili katika upendo,Hekima,na uweza wa Mungu hujipatia amani katika Mungu.Tunaposali tukumbuke mambo matatu.Kwanza Upendo wa Mungu. Ya kuwa Mungu aliye upendo hujibu sala zetu kwa kutujalie mema daima tunayohitaji.Pili Hekima ya Mungu.Mungu mwenye Hekima hutambua yanayotufaa na hayo ndiyo anayotupatia.Na tatu uweza wa Mungu,ya kuwa Mungu aliye Mwenyezi hutujalia yote yanayotufaa,hata yale ambayo hatujaomba.Haifai kufikiri kuwa Mungu hajibu sala zetu.Tuangalie pia yale tunayojaliwa bila hata kuomba.Hayo ndiyo Mungu mwenye upendo,hekima na uweza anaona kuwa yanatufaa.
Tumsifu Yesu Kristo!
Na Padre Augustino Kamnyuka.
Parokia ya Kristo Mfalme Bologna-Italia.
Tarehe 08.10.2017.
No comments:
Post a Comment