WANAFUNZI 18,820 wamekosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza katika Mkoa wa Dar es Salaam mwakani.
Waliofaulu mtihani wa darasa la saba ni 51,488 na wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani ni 32,668 pekee.
Matokeo hayo yalitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Tawala wa Mkoa, Theresia Mmbando, baada ya kikao cha uchambuzi wa wanafunzi hao baina yake na maofisa elimu wa wilaya na mkoa.
Alisema wanafunzi 18,820 wamekosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mwakani wakiwamo wavulana 8,495 na wasichana 10,325 sawa na asilimia 37 ya wanafunzi waliofaulu.
Alisema zipo nafasi 1,246 katika shule za pembezoni ambazo zimebaki kwa sababu ya umbali uliopo kati ya shule hizo zilipo na mahali wanapoishi wanafunzi hao.
Alisema wanafunzi waliobaki wanatarajiwa kuchaguliwa katika chaguo la pili kwa sababu wanafunzi wengi wa Mkoa wa Dar es Salaam hujiunga na shule zisizokuwa za kiserikali.
Kuhusu wanafunzi bora, Mmbando aliwataja wanafunzi 10 bora kwa upande wa wavulana kuwa ni Shaban Mavunde (Tusiime), George Mwapele (Tusiime), George Frank (Tusiime), Ramadhani Juma(Tusiime), Nsajigwa Mwaikambo (Tusiime), Godbless Jumanne (Tusiime), Johnson Sanga (Atlas), Kamselele Mkorwe (Tusiime), Boaz Shonje (Tusiime) na Braun Ntukula (Tusiime).
Aliwatangaza wanafunzi 10 wasichana kuwa ni Justine Gerald (Tusiime), Daniel Onditi (Tusiime), Rachel Ntitu (Atlas), Irene Mwijage (Atlas), Asnath Lemanya (Tusiime), Melisa Mzava (Tusiime), Evermary Mkogwa (Tusiime), Johari Chinemba (Tusiime) na Nelia Ilomo (Tusiime).
Aliipongeza Tusiime kwa kufanya vizuri zaidi katika mtihani huo.
No comments:
Post a Comment