TAFAKARI YA MASOMO YA DOM YA YESU KRISTU MFALME. - KABONGE BLOG.

Blog hii ni kwaajili ya masuala/taarifa za kidini na matukio yanayotokea kila siku.

Breaking

Saturday, November 19, 2016

TAFAKARI YA MASOMO YA DOM YA YESU KRISTU MFALME.

SHEREHE YA BWANA WETU YESU KRISTO MFALME MWAKA C.
MASOMO.

Sam 5: 1 – 3.
Kol 1:11 – 20.
Injili. Lk 23: 35 – 43.

WAZO KUU: HUJACHELEWA BADO KUMGEUKIA NA KUMFUATA KRISTO MFAME.

UTANGULIZI.
Ndug zangu leo ni sherehe ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme. Ni Dominika ya mwisho wa mwaka wa liturujia ya kanisa. Dominika ijayo itakuwa ni Dominika ya  kwanza ya maajilio ambayo ni Dominika kwanza ya mwaka mpya wa kanisa. Tukiwa mwishoni mwa mwaka wa kanisa,Dominika ya mwisho ya kila mwaka sisi wakristo wakatoliki hufanya sherehe ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme. Hutafakari huruma ya mfalme wetu aliyetuongoza katika kuiendea heri ya milele Mbinguni. Mwaka huu, kwa mwaka mzima tulikuwa tunatafakari juu ya huruma ya Mungu. Leo tunahitimisha maadhimisho ya Mwaka wa huruma ya Mungu, uliofunguliwa na Baba Mtakatifu Fransisko tarehe 08. 12. 2015. Masomo yetu leo, yanatutafakarisha kuwa bado hujachelewa kumgeukia Kristo Mfalme. Kama bado hujaanza kumfuata ipasavyo Mfalme wetu, hata kama tunahitimisha mwaka wa huruma ya Mungu, bado hujachelewa,amua sasa kumfuata!
        
UFAFANUZI.
Ndugu zangu, waisraeli walipoingia nchi ya ahadi,kila kabila lilijitawala lenyewe.Ilipotokea vita kati ya Waisraeli na taifa jingine,Mungu alimwinua mtu mmoja kuyaongoza majeshi ya kabila moja  au makabila kadhaa dhidi ya adui.Mtu huyo aliitwa Muamuzi. Katika uongozi huo wa waamuzi waisraeli walikuwa wametawanyika katika vikundi vikundi vya makabila yao bila umoja wa uongozi. Hata hivyo kilichokuwa kinawaunganisha ilikuwa ni kionjo cha kabila lao, na imani yao kwa Mungu mmoja.Baadae waliomba kuingia katika utawala wa kifalme. Walipoingia kwenye utawala wa kifalme baada ya mfalme Sauli, aliingia mfalme Daudi. Daudi alikuwa kiongozi bora aliyewaunganisha makabila yote ya wana wa Israeli kuwa chini ya mfalme mmoja. Somo la kwanza tulilosikia leo linasimulia kuingia na kusimikwa kwa kutiwa mafuta Daudi ili awe mfalme wa makabila yote ya wana wa Israeli. Wazee wote wa Israeli walimwendea Daudi huko Hebron na kumtia mafuta awe mfalme juu ya Israeli.Daudi akawa mfalme wa Israeli yote akiyaunganisha makabila yote chini ya mfalme mmoja. Uongozi wa wafalme uliendelea.Hata hivyo utawala huo wa kifalme  ulianguka baada ya kifo cha mfalme Sulemani na muungano wa makabila uligawanyika na kutengana katika falme mbili.Ufalme wa Yuda  makabila mawili na ufalme wa Israeli makabila kumi.

Katika Injili tumesikia, maneno ya wahalifu wawili waliosulubiwa pamoja na Yesu, Msalabani na maneno ya Yesu kwa mhalifu mmoja. Mmoja kati ya wahalifu hao anamtaka Yesu ajiokoe Msalabani kisha awaokoe na wao. Kumbe mhalifu wa upande wa pili, anamkanya mwenzake na kumuomba Yesu amuokoe si na mateso ya msalabani, bali na adhabu ya milele. Amkumbuke na kumpokea katika ufalme wake. Mhalifu huyo anakiri wazi kuwa Yesu ni mfalme, na mwenye uwezo wote. Halafu tumesikia maneno ya Yesu Kristo akiwa msalabani anamhakikishia mhalifu aliyeomba kukumbukwa katika ufalme wake, kuwa atakuwa nae mahali pema peponi.Ni dakika za mwisho kabisa yule mhalifu alimgeukia Yesu,  akapata wokovu.

Katika somo la pili Mtume Paulo anasali akimshukuru Mungu kwaajili ya wakolosai. Anamshukuru Mungu kwa mambo makuu mawili ambayo Mungu anawatendea wakolosai. Kwanza Mungu  amewastahilisha wakolosai kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu wa Mungu.Pili amewahamisha wakolosai na kuwaingiza katika ufalme wa mwanae mpenzi. Kwa kuwaingiza katika ufalme huo wa mwanae ilikuwa ni ukombozi toka gizani na kuingia nuruni, toka utumwani na kuingia kwenye uhuru, toka kwenye laana na kuingia kwenye msamaha, na toka kwenye nguvu za shetani na kuingia kwenye nguvu za Mungu.
MAISHANI.

Ndugu zangu tupo mwishoni mwa mwaka wa liturujia ya kanisa na tupo kwenye kilele cha mwaka wa huruma ya Mungu. Leo kanisa duniani pote linahitimisha maadhimisho ya mwaka wa huruma ya Mungu. Tuelewe kuwa kanisa kamwe halifungi huruma ya Mungu. Huruma ya Mungu haina mipaka, na hivyo hata wale ambao bado hawajafaulu kumgeukia Kristo mfalme kwa mwaka huu wajue kuwa bado hawajachelewa kumgeukia na kumfuata. Bado ipo nafasi kama ya yule mhalifu aliye sulubiwa pamoja na Kristo aliyemgeukia Kristo muda mfupi kabla ya kifo chake. Ni mhimu sana kumgeukia, kumsikiliza, kumtii na kumfuata mfalme, kiongozi wetu bora,Bwana wetu Yesu Kristo; kwasababu;

Kwanza ni Mfalme mwenye uwezo wote: Ingawa Yesu alikuwa na uwezo wa kushuka msalabani, hakushuka; ili kitendo chake cha kubaki msalabani kituletee msamaha na wokovu sisi wote. Kama angelishuka kutoka msalabani angekuwa ameusaliti utume wake wa kuwafikisha watu kwa Mungu. Kwa kitendo cha kumuahidi mhalifu mahali pema peponi kinathibitisha kuwa Yesu ana uwezo wa kuokoa hata kama hajiokoi mwenyewe msalabani.Hujachelewa kumgeukia na kumfuata Mfalme mwenye uwezo wote.Fanya hima sasa,yeye ni Mwenyezi!

Pili; Kristo ni Mfalme mwenye huruma. Huruma ya mfalme huyu haina mipaka. Anasamehe na kuwahurumia wote wanaomsadiki hata dakika ya mwisho ya maisha yao ya hapa duniani. Kamwe usione umechelewa kumgeukia na kumfuata Kristo. Bado ipo nafasi ya huruma yake. Huruma yake haina mipaka. Tuamuke na kumtazama yeye waliyemchoma. Hujachelewa bado kumgeukia na kumfuata Mfalme mwenye huruma.Fanya hima sasa,huruma yake ni ya milele!
Tatu; Kristo ni Mfalme mshindi. Wayahudi walidai Yesu asulubiwe Msalabani na siyo kumpa adhabu nyingine maana adhabu ya kusulubiwa msalabani ilikuwa ni ya mateso makali na aibu kubwa. Tena kufa juu ya msalaba (mti) kulitazamwa kuwa ni laana toka kwa Mungu (Kumb 21:23, Gal 3:13). Wayahudi walitaka Yesu Kristo apate mateso hayo makali na kuonekana kuwa amekataliwa na kulaaniwa na Mungu. Ushindi wa Yesu kwa kufufuka kwake ulipindua mawazo hayo yote. Ni Yesu Kristo aliyeshinda. Mkristo ajue kuwa Kristo Mfalme wake, ni mshindi asikate tamaa katika changamoto na magumu yake kwa kuwa anaye Kristo mshindi anayeyaongoza maisha yake kwenye ushindi. Hujachelewa bado kumgeukia na kumfuata Mfalme mshindi.Fanya hima sasa,yeye ni Kristo mshindi!

Nne; Kristo Mfalme ni kiongozi na msimamizi wetu.Hivi tunapaswa kuwa waaminifu kwake.Ni Mfalme anayetulinda dhidi ya maadui wanaotushawishi tutende mabaya.Anatulinda kwa kutuonehsa njia salama na kutupatia neema ya kufaulu kupita katika  njia hiyo.Mfalme wetu anatustawisha kwa kutuongza katika wajibu zetu.Anatuongoza kushika kiaminifu agano letu na Mungu. Leo tunamshangilia Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme,ambaye aliibuka na ushindi dhidi ya dhambi na kifo.Tukubali ayaongoze maisha yetu.Tusilegee kimsimamo kufuata mafundisho yake. Tunampenda Yesu,tumebatizwa kwa jina lake, tuondokane na vitendo vya kumkaidi Yesu Kristo Mfalme wetu, badala yake tukaze nia ya kuishi kama wafuasi wake.

HITIMISHO.
Ndugu zangu, leo tunahitimisha mwaka wa huruma ya Mungu. Lakini tusisahau kuwa kwa kuongozwa na Mfalme wetu mwenye huruma lazima tuendelee kupigana kwa dhati na shetani na wafuasi wake, kwa kutumia uhuru wetu katika kuwahudumia wenzetu ili sote tufaulu kuufikia uungwana wa wana wa Mungu. Kamwe hujachelewa! Lakini muda wake ndio sasa, kamwe usichelewe kwa kujichelewesha! Fanya hima!

Tumsifu Yesu Kristo!
Na Padre Augustino Kamnyuka.
Parokia ya Ulete,20.11.2016.

No comments:

Post a Comment