TABORA YAONGOZA KWA WANAFUNZI HEWA. - KABONGE BLOG.

Blog hii ni kwaajili ya masuala/taarifa za kidini na matukio yanayotokea kila siku.

Breaking

Wednesday, November 9, 2016

TABORA YAONGOZA KWA WANAFUNZI HEWA.

Serikali imefanikiwa kuokoa Sh. 931,317,500 baada ya kushitukia kuwapo kwa wanafunzi ‘hewa’ katika shule za msingi na sekondari nchini katika mwaka wa fedha 2016/17.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, akizungumza na wanahabari mjini Dodoma alisema fedha hizo zimeokolewa baada ya zoezi la uhakiki lililoanza Agosti 18, mwaka huu, lililofanywa na makatibu tawala wa mikoa yote Bara.

Simbachawene amesema kiasi hicho kimeokolewa baada ya kufanyika zoezi hilo na kubainika kuwapo wanafunzi ‘hewa’ 52,783 wa shule za msingi na sekondari walipatikana 12,415.

Alisema zoezi hilo la uhakiki lilifanywa na makatibu tawala baada ya kuagizwa na Tamisemi kulinganisha na taarifa ya Machi, mwaka huu, wakati wa ujazaji wa madodoso ya takwimu za shule za awali (TSA) na nyaraka za mahudhurio ya wanafunzi.

“Idadi ya wanafunzi kabla ya uhakiki huo Machi mwaka huu, kulikuwapo na wanafunzi 9,746,534 wa shule za msingi na 1,483,872 wa sekondari, lakini baada ya uhakiki huo, ilibainika kuwapo wanafunzi wa shule za msingi 9,690,038 na sekondari 1,429,314,” alisema Simbachawene.

Waziri huyo alisema kati ya fedha zilizookolewa iwapo zingetumika kuwagharamia wanafunzi hao, Sh. 527,830,000 zingetakiwa kutumika kwa shule za msingi na 403,487,500 kwa shule za sekondari.
Hata hivyo, alisema hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa wakuu ambao watabainika kusababisha kuwapo kwa wanafunzi hewa.

Aidha, Simbachawene alisema mkoa wa Tabora ndiyo ulioongoza kwa kuwapo na wanafunzi hewa wengi huku wale wa shule za msingi wakiwa 6,985 na 5,127 sekondari jumla wakiwa 12,112.

Simbachawene alisema mkoa uliofuata ni Ruvuma jumla ya wanafunzi hewa 7,743, Mwanza (7,349), Dar es Salaam (4,906), Kagera (4,763), Rukwa (4,054), Singida (3,239), Kilimanjaro ((2,594), Kigoma (2,323) na Njombe 2,307.

Mikoa mingine ni Simiyu (2,081), Arusha (1,923), Mara (1,855), Tanga (1,378), Geita (1,281), Morogoro (1,172), Mtwara (882), Mbeya (786), Shinyanga (695), Songwe (512), Manyara (330), Dodoma (284), Lindi (281), Pwani (187), Iringa (161) na Katavi (0).

No comments:

Post a Comment