SERIKALI imeagiza kukamilika mapema kwa mfumo wa udahili wa vyuo vikuu ili mapendekezo yatakayokuwa na mfumo wenye tija yaweze kuingizwa wakati wa maandalizi ya bajeti ya mwaka 2017/2018.
Hatua hiyo ni katika kutatua changamoto zinazojitokeza katika uratibu wa mikopo ya wanafunzi na kwamba Serikali inafanya mapitio ya mfumo wa udahili wa wanafunzi, utaratibu mzima wa utoaji na urejeshaji wa mikopo kwa lengo la kuwa na mfumo bora na kuondoa adha inayowapata wanafunzi wanapofungua vyo kutokana na mfumo wa sasa.
Hayo yameelezwa katika hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya kuahirisha mkutano wa Bunge, ambapo juzi hakuweza kutoa hotuba ya kuahirisha Bunge na badala yake alitoa hoja ya kuahirisha huku akitaka hotuba yake iingiwe katika kumbukumbu rasmi za Bunge.
Hotuba haikusomwa kutokana na kifo cha ghafla cha Mbunge wa Dimani, Hafidh Ali Tahir (CCM) aliyefariki wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Katika hotuba hiyo alisema hadi kufikia Novemba 2, mwaka huu jumla ya wanafunzi 25,228 wa mwaka wa kwanza walikuwa wameshapewa fedha za mikopo, huku kati yao 4,787 ni yatima, 127 wenye ulemavu na 94 waliosoma sekondari kwa ufadhili wa taasisi mbalimbali.
“Nimeagiza kazi hii ikamilike mapema ili mapendekezo ya mfumo utakaokuwa na tija zaidi yaweze kuzingatiwa wakati wa maandalizi ya bajeti ya 2017/18,” alisema Majaliwa.
Pamoja na hayo, pia Waziri Mkuu aligusia masuala mengine ikiwemo maafa ya Kagera, sekta ya kilimo, uchumi na viwanda, nishati pamoja na sekta zingine.
No comments:
Post a Comment