BUNGE limenusa ufisadi katika Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali baada ya kubaini kuna mashine ya uchapaji ilinunuliwa kwa gharama kubwa, ikafanya kazi kwa muda mfupi na mpaka sasa, haifanyi kazi.
Aidha, Bunge limebaini ofisi hiyo haina usiri wa nyaraka za serikali zinazochapwa kwa kuwa baadhi ya nyaraka zinachapwa nje ya ofisi na inajiendesha chini ya viwango.
Waliishauri Serikali ifanye mabadiliko ya Menejimenti kwa kuwa muda mrefu hakuna ufanisi, taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo ilieleza hayo.
Taarifa hiyo iliridhiwa na Bunge bila kujadiliwa na wabunge juzi wakati Mwenyekiti wake, Andrew Chenge alipokuwa akifanya majumuisho mafupi bungeni mjini hapa.
Taarifa hiyo iliwasilishwa Alhamisi, Novemba 10 na Makamu Mwenyekiti wa kamati na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM) lilipaswa kujadiliwa juzi lakini haikuwezekana kutokana na kifo cha Mbunge wa Dimani, Hafidh Ali Tahir (CCM) kilichotokea ghafla usiku wa kuamkia juzi mjini hapa.
Pia shughuli za Bunge ziliahirishwa mara mbili katika Mkutano huo wa Tano wa Bunge la 11, kutokana na kifo cha Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta.
Akiwasilisha taarifa hiyo ambayo ilifanyiwa majumuisho mafupi na Chenge juzi, Ngeleja alisema Kamati hiyo ilifanya ziara katika Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Machi 15 mwaka huu na kujionea shughuli za ofisi hiyo za uchapaji wa nyaraka za serikali, zikiwemo Sheria Ndogo.
“Hata hivyo Kamati hii imebaini kuwa Idara hii haiendeshwi kwa viwango vinavyokidhi mahitaji yaliyopo. Kwa mfano katika vikao vya Kamati vilivyopita, Kamati haikupokea kwa wakati Sheria Ndogo mbalimbali kwa sababu hazikuwa zimechapwa na Mpiga Chapa wa Serikali,” alisema Ngeleja.
Kamati hiyo ilisema kuwa dosari hiyo inatokana na ukweli kwamba ofisi hiyo inatekeleza majukumu yake chini ya kiwango kinachotakiwa na iko nyuma kiteknolojia.
“Kamati haikuridhishwa na maelezo ya Menejimenti ya Idara hiyo kuhusu uendeshaji na utendaji kazi na pia haikuridhishwa na hatua ya idara hiyo kutumia fedha za umma kununua mashine ya uchapaji kwa gharama kubwa na mashine hiyo kufanya kazi kwa muda mfupi… kamati inashangaa kwa nini hadi wakati Kamati inafanya ziara hiyo, mashine hiyo ilikuwa haifanyi kazi,” alisema Ngeleja bila kueleza ni kiasi gani kiligharimu manunuzi ya mashine hiyo.
Ngeleja alisema kamati ilibaini pia kuwa, kazi nyingi za idara hiyo zinafanywa nje ya idara kwa sababu printa ya ofisi hiyo huzidiwa na kazi.
“Kwa kutoa kazi hizo nje, kazi huchelewa lakini pia inapoteza usiri wa nyaraka za serikali na fedha nyingi kupotea,” alisema na kuongeza kuwa Kamati hiyo iliishauri serikali kuchukua hatua za haraka kuiboresha idara hiyo ili iachane na tabia ya kuchapisha nyaraka za serikali nje ya ofisi hiyo kwani inahatarisha usalama wa nyaraka na kuongeza gharama.
Maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria katika taarifa yake kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ilishauri pia kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu iboreshe mitambo na mazingira ya Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kuiwezesha kufanya shughuli zake kibiashara zaidi.
Kamati ya Sheria Ndogo katika ziara yake ilibaini pia kuwa mitambo ya Idara hiyo ni chakavu, majengo yaliochini ya kiwango pamoja na uhaba mkubwa wa vitendea kazi na kuishauri serikali, menejimenti ya Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ifanyiwe mabadiliko kwa sababu kwa muda mrefu imekuwa haitekelezi majukumu yake kwa ufanisi.
Imeshauri pia maslahi na mazingira ya kazi kwa watumishi wa ofisi hiyo yaboreshwe ili kuendana na shughuli wanazozifanya. Akifanya majumuisho ya taarifa hiyo juzi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge aliitaka Serikali ifanyie kazi mapendekezo hayo ya Kamati ili kuboresha maeneo yaliobainishwa kuwa na changamoto.
No comments:
Post a Comment