Robo Fainali ya tatu ya Kombe la Shirikisho la TFF kati ya Azam FC na Ndanda FC inafanyika leo Aprili 5, 2017 saa 1.00 usiku kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Kuelekea mpambano huo, timu zote mbili zimetambiana kuibuka na ushindi, huku Azam ikitaka kutofanya makosa katika michuano hii ili ijihakikishie nafasi ya kushiriki katika michuano ya kimataifa msimu ujao.
Ndanda FC kutoka mkoani Mtwara ni moja kati ya timu ambazo huipa wakati mgumu Azam pindi zinapokutana hasa katika michezo ya ligi, ambapo katika mechi ya mzunguko wa pili Azam walishinda bao 1-0 wakilipa kipigo cha mabao 2-1 walichokipata katika mchezo wa mzunguko wa kwanza.
Tayari timu za Mbao FC ya Mwanza na Simba ya Dar es Salaam, zimefuzu kwa hatua ya Nusu Fainali. wakati Robo Fainali ya nne na ya mwisho kati ya Young Africans na Tanzania Prisons FC ikipangwa kufanyika Aprili 22, 2017 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Bingwa wa michuano hi ambayo msimu huu ilishirikisha timu 86 ikiwa ni pamoja na za Ligi Kuu (timu 16); Ligi Daraja la Kwanza (timu 24); Ligi Daraja la Pili (timu 24) na mabingwa wa mikoa timu 22, atawakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho - CAF.
No comments:
Post a Comment