MASOMO YA DOMINIKA YA 7 YA MWAKA A WA KANISA. - KABONGE BLOG.

Blog hii ni kwaajili ya masuala/taarifa za kidini na matukio yanayotokea kila siku.

Breaking

Saturday, February 18, 2017

MASOMO YA DOMINIKA YA 7 YA MWAKA A WA KANISA.

MASOMO YA MISA, FEBRUARI 19, 2017
DOMINIKA YA 7 YA MWAKA A WA KANISA
WIMBO WA MWANZO:
Zab. 13:5 – 6
Nami nimezitumainia fadhili zako; moyo wangu na uufurahie wokovu wako. Naam, nimwimbie Bwana, kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu.
SOMO 1
Law. 19:1 – 2, 17 – 18
Bwana alinena na Musa, akamwambia, Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu. Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi Bwana.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 102:1 – 4, 8, 10, 12 – 13
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
Ee nafsi yangu umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyomo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote. (K)
Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema, (K)
Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Hukutenda sawasawa na hatia zetu,
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. (K)
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake,
Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao. (K)
SOMO 2
1Kor. 3:16 – 23
Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.
Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ilia pate kuwa mwenye hekima. Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye awanasaye wenye hekima ktika hila yao. Na tena, Bwana anayafahamu mawazo ya wenye hekima ya kwamba ni ya ubatili. Basi, mtu yeyote na sijisifie wanadamu. Kwa maana vyote ni vyenu; kwamba ni Paulo, au Apolo, au Kefa; au dunia, au uzima, au mauti; au vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu; nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.
SHANGILIO
Yn. 14:23
Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu, na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake.
Aleluya.
INJILI
Mt. 5:38 – 48
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo. Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru; je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

No comments:

Post a Comment