WAZIRI AAGIZA SHULE NA MAJESHI KUACHA KUTUMIA KUNI. - KABONGE BLOG.

Blog hii ni kwaajili ya masuala/taarifa za kidini na matukio yanayotokea kila siku.

Breaking

Tuesday, November 29, 2016

WAZIRI AAGIZA SHULE NA MAJESHI KUACHA KUTUMIA KUNI.

<
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka taasisi za serikali zinazotumia kuni na mkaa kwa wingi kama vile shule na majeshi kuanza mikakati madhubuti ya kubadili mfumo wa kupikia na kuweka majiko ya gesi ili kupunguza matumizi ya mkaa ambayo yamekuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.
Alisema hayo jana Dar es Salaam katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe wakati wa ufunguzi wa warsha ya wadau kujadili namna na njia bora ya kupunguza matumizi ya mkaa kwa usimamizi endelevu wa mazingira nchini.
“Nimeelezwa kuwa makampuni yanayouza majiko na gesi ya kupikia aina ya LPG yameonesha nia ya kuweka majiko haya bila gharama yoyote. Tutumie vyombo vyetu vya habari na majukwaa ya mikutano kuhamasisha wananchi kutumia fursa hii ya LPG,” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, alisema nchi inakabiliwa na changamoto kubwa za uharibifu wa mazingira kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ufugaji wa kuhamahama, mifugo kuvamia misitu na kuiharibu pamoja na vyanzo vya maji na watu kukata miti katika vyanzo hivyo.
Alisema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha mabadiliko ya vipindi vya mvua, mtawanyiko wa kiwango cha mvua na hivyo kutishia usalama wa chakula na ukosefu wa malighafi kwa viwanda ambavyo ndiyo njia ya kuivusha nchi kuingia katika uchumi wa kati.
Alisema takwimu zinaonesha asilimia 90 ya nishati ya kupikia hasa mijini ni mkaa na kwa vijijini asilimia kubwa na wananchi wanatumia kuni ambapo takwimu hizo pia zinaonesha ili kuzalisha tani moja ya mkaa sawa na magunia 30 zinahitajika tani 12 za kuni na hali hiyo imesababisha nchi kupoteza zaidi ya hekta 370,000 kila mwaka.
Alisema utafiti pia umebainisha kwamba matumizi ya mkaa yanaongezeka kutokana na ongezeko la watu na kama haitaanza kutumika nishati mbadala, mahitaji ya mkaa yatafikia takribani tani milioni tano kwa mwaka ifikapo mwaka 2030 kutoka tani milioni 2.4 zilizotumika mwaka 2015.
Hata hivyo, Profesa Maghembe alisema wizara yake inatarajia kupandisha ushuru na kodi ya mkaa ili uuzwe kwa bei ya juu lengo likiwa ni kuwafanya wasafirishaji na wanunuzi washindwe kumudu gharama na hatimaye matumizi ya mkaa kupungua.



No comments:

Post a Comment