HAPI ATAKA MWALIMU MKUU WA MWANANYAMALA KUSHUSHWA CHEO. - KABONGE BLOG.

Blog hii ni kwaajili ya masuala/taarifa za kidini na matukio yanayotokea kila siku.

Breaking

Tuesday, November 1, 2016

HAPI ATAKA MWALIMU MKUU WA MWANANYAMALA KUSHUSHWA CHEO.

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Aron Kagurumjuli kumshusha cheo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwananyamala B, Emmanuel Temba kwa makosa mbalimbali, ikiwemo kufanya biashara shuleni.

Akitoa agizo hilo katika ziara ya kutembelea kata za manispaa hiyo jana, Hapi alisema ametoa adhabu hiyo kwa kosa la kufanya biashara ya vibanda shuleni hapo wakati agizo la serikali lililotolewa mwaka 2006, haliruhusu biashara shuleni.

‘’Huyu mwalimu mkuu wa shule hii, hatufai haiwezekani afanye biashara ya vibanda shuleni wakati serikali ilishakataza huku akiwaruhusu wafanyabiashara kutumia vyoo vya watoto wetu wanaosoma hapa, na kuagiza mkurugenzi mvue cheo huyu mwalimu,” alisema Hapi.

Aidha, Hapi alisema kosa lingine linalomkabili Temba ni kuruhusu wafanyabiashara wa vibanda hivyo kutumia vyoo vya wanafunzi vilivyopo shuleni hapo, ikiwa ni pamoja kuweka kituo cha kuuza mafuta ya taa katika eneo la shule. Hapi alitoa agizo hilo huku mwalimu mkuu huyo akiwa hayupo shuleni hapo, na taarifa zilidai alienda kwenye msiba wa kaka yake.

Mkuu huyo wa wilaya alitembelea pia Soko la Mwananyamala Kisiwani ambako aliagiza ujenzi wa soko hilo uliosimama kwa muda mrefu uanze.

“Hili soko haiwezekani fedha zimeshatolewa na Halmashauri, lakini ujenzi mpaka leo haujaisha, nawapa wiki mbili ujenzi uanze mara moja,” alisema.

Na, Paschal Kabonge.

No comments:

Post a Comment