AGIZO LA JPM LAMTESA 'DC' AAMUA KUJIACHIA. - KABONGE BLOG.

Blog hii ni kwaajili ya masuala/taarifa za kidini na matukio yanayotokea kila siku.

Breaking

Tuesday, November 22, 2016

AGIZO LA JPM LAMTESA 'DC' AAMUA KUJIACHIA.

Licha ya kuwapo kwa agizo la Rais John Magufuli kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kutoomba chakula cha msaada serikalini, Mkuu wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Lyidia Bupilipili amesema hana jinsi, lazima aombe ili kuwanusuru wananchi kufa kwa njaa.


Mapema katika maagizo yake, Rais Magufuli aliwahi kuwazuia wakuu hao kuomba chakula cha msaada badala yake wawasimamie wananchi katika maeneo yao ili wazalishe kwa wingi.

Hata hivyo, Bupilipili alidai ni vigumu kwa hali iliyojitokeza katika wilaya yake kukaa kimya bila kupaza sauti ya kuomba msaada wa chakula.

Akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha, mkuu huyo wa wilaya alisema ili kunusuru uhai wa wananchi ombi lake la msaada linapaswa kutekelezwa.

Aliongeza kuwa sanjari na ombi hilo anaiomba Serikali iwauzie wananchi hao kwa bei nafuu ili waweze kumudu kununua chakula hicho.

Bupilipili alisema hayo wakati akimkaribisha naibu waziri huyo kuzungumza na wananchi kuhusu migogoro ya ardhi baina ya wakazi wanaopakana na hifadhi za wanyama.

Alisema wilaya hiyo inakabiliwa na njaa kali huku baadhi ya familia zikikumbwa na utapiamlo na kwamba mahitaji ya chakula ni zaidi ya tani 163.6.

“Sababu zilizochangia wilaya kukosa chakula ni tembo kuharibu mazao mashambani na kuvamia vyakula vilivyohifadhiwa katika maghala na kula vyote,” alisema Bupilipili

Akijibu ombi hilo, ole Nasha alisema atahakikisha chakula cha msaada kinawafikia wananchi mapema iwezekanavyo na kwamba amekwisha kupokea ombi kama hilo kutoka kwa Mkuu wa mkoa huo, Dk Charles Mlingwa.

No comments:

Post a Comment