MASWALI SITA KUHUSU KUTESWA HADI KUFA KWA YESU. - KABONGE BLOG.

Blog hii ni kwaajili ya masuala/taarifa za kidini na matukio yanayotokea kila siku.

Breaking

Thursday, April 13, 2017

MASWALI SITA KUHUSU KUTESWA HADI KUFA KWA YESU.

IJUMAA KUU - KUFA KWA YESU

Kifo cha Yesu, kilitanguliwa na kilio ambacho kilikuwa katika mfumo wa swali: "Eloi, Eloi, lama sabakthani?" (rej. Zab 22:1) Maana ya kilio na swali hili ni Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha? Kristo alilia na kuuliza hivyo, kwa sababu kama binadamu alijisikia kuachwa na Mungu.

Kilio cha Yesu kinatujulisha hisia yake ya kuachwa na wala haizungumzii kukata tamaa. Kukata tamaa ni mbali na kuhisi kuwa umeachwa peke yako katika shida. Katika umungu wake, kwa vyovyote hakubandukana na Mungu na ndiyo maana hakutenda dhambi.

Tunasema hivyo, kwa sababu dhambi ni kuvunja uhusiano na Mungu na kwa Kristo, inajulikana kwamba Kristo alijaribiwa kam binadamu wote, isipokuwa hakufanya dhambi (Ebr 4:15)

Wayahudi waliposikia Yesu akitamka "Eloi, Eloi" walipotea katika kuelewa lugha yao wenyewe, yaani Kiaramayo. Wao waliruka kimawazo na kudhani Yesu alikuwa akimwita nabii Eliya aje.

Kwa nini kulitokea mruko huo wa kimawazo? Sababu ni mbili:

·  Mosi Wayahudi waliokuwa wakishuhudia kifo cha Yesu pale chini ya msalaba,

o   Waliharibikiwa vichwa kwa ukatili wao.

o   Walikuwa na vichwa vilivyokosa utulivu. Katika hali hiyo, walishindwa kufuatili vyema maneno ya adui yao.

·  Pili, mruko huo ulisababishwa na imani ya Kiyahudi kwamba, Nabii Eliya ni msaidizi wa watu wote walio taabuni. Hivyo, Yesu alipotamka Eloi, Eloi wao wakafikiri kwa mruko kwamba, Yesu alikuwa akimwita Eliya, msaidizi wa walio taabuni aje amsaidie katika mateso yake makali pale msalabani

Tukumbuke tena kwamba, Wayahudi wanamsubiri sana Eliya, kwani anapaswa kuja kabla ya kuja kwake Masiha (rej. Mal 3:23, Mt 11:14, 17:10-11, Mk 9:11-12).

·Ni kawaida iliyojengeka hadi leo hii, kwa Wayahudi kutofunga mlango wakati wanapokula chakula, ili Eliya aingie akitaka na pia wanasadiki kwamba, mbwa anapobweka amemwona au amemnusa Eliya mahali hapo.

Baada ya kilio chake, Yesu aliutangazia ulimwengu kwamba, alikuwa ameimaliza kazi aliyotumwa na Baba yake. Ndipo akamkabidhi Baba yake roho yake (rej. Yn 19:30). Maneno anayosema Yesu kufani kwake na jinsi anavyomkabidhi Baba yake roho yake, vyote vinaonesha kwamba Yesu alikipokea kifo chake kwa hiari ya moyo wake. Katika mateso kulalamika siyo hoja, kwani hilo ni jambo la kibinadamu. Tuusome moyo. Moyo ndiyo hasa wenye kuonesha kama kuna hiari au la.

KUPASUKA KWA PAZIA LA HEKALU

Pazia la hekalu lilikuwa pazia la ndani ya hekalu. Wala halikuwa pazia la dirisha fulani tu, bali pazia la mahali rasmi kabisa. Lilikuwa kati ya Patakatifu na Patakatifu pa Patakatifu. Yaani, kati ya Patakatifu na Patakatifu pa Patakatifu hapakuwepo mlango wo wote, isipokuwa pazia lenye darizi. Darizi ilikuwa ya picha za viumbe vyenye mabawa (rej. Kut 26:31).

Patakatifu ndipo mahali alipoingia kuhani wa zamu kila siku, ili kutolea sadaka ya uvumba kwenye altare ya uvumba, iliyokuwemo humo ndani. Humo humo, kulikuweko meza yenye mikate kumi na miwili ya mwonesho. Mikate hiyo ilipobadilishwa, makuhani peke yao waliruhusiwa kuila. Tena humo humo, kulisimama kinara (menorah) cha taa saba ambazo daima zilikuwa zikiwaka.

Patakatifu pa Patakatifu, ndipo mahali palipokuwa patakatifu kupita sehemu zote. Hapo mwanzoni, paliwekwa Sanduku la Agano, ambalo ndani yake kuliwa na

·        Mbao mbili za Amri Kumi za Mungu,
·        Chungu kidogo chenye manna ndani pamoja na
·        Fimbo ya Musa au Haruni.

Sanduku la Agano na kiti chake cha huruma juu yake, ndilo lililowakilisha uwepo wa Mungu humo hekaluni na katika mji wa Yerusalemu kwa ujumla.

Utakatifu wa hekalu, ulitokana na Sanduku la Agano. Kutokana na kuchukuliwa huku na huko hasa wakati wa vita, sanduku la Agano lilipotea na halijulikani liliko hadi leo hii. Kuna habari kwamba, liko huko Ethiopia kati ya watu wenye asili ya Kiyahudi wakaao huko.

Lakini habari hii ni ngumu kuhakikishwa, kwa sababu kuna mifano mingi ya Sanduku la Agano iliyotengenezwa na zaidi ya hayo, lile sanduku linalosemekana kuwa la asilia hakuna aliyepata kuruhusiwa kwenda kuliona, maana linalindwa kila mara na mtu mwenye hadhi ya ukuhani tu. Watakaokujua ukweli, waende wenyewe huko Ethiopia.

1. KWA NINI PAZIA LA HEKALU LIPASUKE WAKATI WA KIFO CHA YESU?

Msingi wa jibu kwa swali hili, upo kwenye ukweli kwamba, kifo cha Yesu kilikuwa ni kifo cha sadaka ya ukombozi. Hivi, ili kuutangazia ulimwengu jambo hili, Mungu alifanya muujiza wa kulipasua pazia la hekalu wakati Yesu alipokuwa akifa kisadaka.

Ndipo basi, kiteolojia maana ya kupasuliwa kwa pazia la hekalu, ni kuashiria kuanza kwa enzi mpya ya historia ya wokovu. Yaani, katika enzi hiyo mpya, hekalu halitakuwa na umuhimu wo wote wa pekee, kwa vile sadaka itakuwa ni moja tu, yaani ya Yesu na Mungu atakuwa mioyoni mwa watu, kwani Mungu atajulikana kuwa ni roho mwenye kuabudiwa rohoni.

2. YESU ALISULIBIWA SAA NGAPI?

Injli zetu nne zinaonekana kusigana juu ya saa ya kusulibiwa na kufa kwa Yesu Kristo. Msigano wenyewe usitubabaishe. Kwa ujumla, wainjili watatu waliotuandikia Injili ndugu, yaani Matayo, Marko na Luka, wanaonesha kwamba

·Yesu alisulibiwa mnamo saa tatu asubuhi.
· Ilipofika saa sita mchana kukaanza kuingia giza na
· Ilipofika saa tisa, akaikabidhi roho yake mikononi mwa Baba yake.
· Mwinjili Yohane peke yake, anasema Yesu alichukuliwa kwenda kusulibiwa mnamo saa sita na hivi basi, alikufa baada ya saa sita.

Tuseme nini katika msigano huu? Msigano huu umesababishwa na tofauti ya malengo ya kiteolojia yaliyokuwa tofauti kati ya Yohane na wainjili wa Injili ndugu.

· Yohane alipokuwa akiwajibu watu waliokuwa wanamdadisi juu ya kifo cha kisadaka cha Yesu, alijitahidi kuwaeleza kwamba, Yesu alijitoa sadaka kama mwanakondoo wa Pasaka.

·  Kumbe, wale Wainjili ndugu hawakuwa na lengo kama hili, ndipo waliporipoti kile kilichotokea tu.

Kwa mwono wake Yohane, ndipo alipoanza hata kwa kuonesha kuwa aliuawa siku ya kuandalia Pasaka. Ndipo basi, mlo aliokula Yesu kabla ya kifo chake, ulikuwa ni mlo wa mwisho tu,

·        Wakati Wainjili wenzake wanasimulia mlo huo wa mwisho ulikuwa pia mlo wa Kipasaka.

Mradi wa kumwonesha Yesu kama mwanakondoo, haukuanzia katika masimulizi ya mateso tu, bali umeanzia katika sura za mwanzo za Injili yake. Tunasoma kwanza, katika 1:29 pale ambapo alimwonesha Yesu kwa watu, kwa kumwita mwanakondoo aondoaye dhambi za dunia. Ndipo ilipofika saa ya mateso au utukufu wa Yesu, akatupangia mambo kwa mtindo wa pekee, ili yaoane na kauli kwamba Yesu alikuwa mwanakondoo wa sadaka.

Ndipo basi, anaanza kwa kusema, Yesu alichukuliwa kwenda kusulibiwa saa zile zile, ambapo wanakondoo wa Pasaka walipokuwa wakipelekwa kuchinjwa huko hekaluni na hivyo kufa kwake, kulitokea saa zile zile, walipokuwa wakichinjwa wanakondoo wa Pasaka huko hekaluni. Yaonekana kwamba teolojia ya Yesu kama mwanakondoo, ilitawala sana kambi ya Yohane, ndipo teolojia hiyo inapojitokeza tena katika kitabu cha mwisho cha Biblia, yaani Ufunuo wa Yohane.

3. MAHAKAMA GANI ILIMHUKUMU YESU? IJUMAA KUU

Mahakama iliyomhukumu Yesu ilikuwa ya wakoloni, yaani Warumi ambao walikuwa wanawatawala Wayahudi, kwa njia ya Gavana wake aliyewekwa mjini Kaesaria Maritima. Wakati ule wa Yesu, Gavana wa kirumi alikuwa ndiye Pontio Pilato. Lakini, ijapokuwa tunasema Pilato kama Gavana wa Kirumi, ndiye aliyesema kwa amri ya mwisho achukuliwe Yesu na wakamtendee watakavyo, kwa kweli alishinikizwa na Wayahudi na wakuu wao, maana hao walihakikisha Yesu anauawa hata kwa kumtisha Pilato.

Na kweli, Pilato alitishiwa kushtakiwa kwa Kaisari, yaani Mfalme Mkuu wa dola ya Kirumi kwa kumwachilia mtu kama Yesu, anayejiita mwenyewe Mfalme, wakati mfalme ni mmoja tu, Kaisari. Matisho kama haya, pamoja na kelele za "Msulibishe, Msulibishe", yalimshinikiza Pilato aamue Yesu achukuliwe na akatendewe kwa kadiri Mayahudi walivyotaka.

Mashtaka ya mwisho, Pontio Pilato aliandika kibaoni kuwa, ni kujiita Mfalme wa Mayahudi. Walipomburura msulibiwa kuelekea mahali atakakosulibiwa, mvulana mdogo alipewa kibao cha mashtaka na kutangulia nacho mbele ya waandamanaji, kusudi kama kuna mtu haungi mkono mashtaka yale, ayasimamishe maandamano na kuwarudisha wote mahakamani kwa ajili ya kuisikiliza kesi upya.

Kwa mashtaka ya Yesu, wapo waliotaka kupinga mashtaka yale kwa kufanyiwa marekebisho kidogo, lakini siyo kuyafuta kabisa mashtaka yale. Walitaka Pilato aandike kwamba, Yesu mwenyewe alisema kwamba yeye ni Mfalme wa Wayahudi. Pilato alikataa kufanya mabadiliko hayo, maana alishapotoshwa kabla hajaandika kibao kile (Yn 19:22).

  4. MATESO GANI ALIFANYIWA MTU ALIYESULIBIWA?

Kabla hatujaendelea mbele, tuseme kwanza neno moja. Yaani, tuseme kwamba kwa kadiri ya sheria ya kirumi na ile ya kiyahudi, mtu wa kuuawa ilibidi akauawe mara baada ya hukumu kutolewa. Hii ndiyo sababu Yesu alitolewa haraka haraka, kwenda kusulibiwa. Wakati ule, waliohukumiwa kuuawa hawakupata muda tena wa kusubiri kifo, kama inavyotokea katika sheria za leo.

Ingawa kesi iliendeshwa ndani na daima kwenye makao makuu ya mtawala (rej. Mt 27:27),

·  Kusulibiwa kwenyewe kulifanyika nje ya mji,

·  Kwenye sehemu ya makutano ya njia,

·  Kusudi watu wengi kwa kadiri ilivyowezekana, wamwone aliyesulibiwa na wapate kutishika kwa tukio lile.

·  Basi, ndivyo ilivyofanyika katika kumsulibisha Yesu kilimani Golgota. Wayahudi wenyewe walipompa mtu adhabu ya kifo, walimuua kwa kumpiga mawe watu wengi kwa pamoja. Kishapo, ndipo walipomtundika mtini.

Lakini, Warumi walikuwa na mtindo wa peke yao.

·  Wao waliwasulibisha watu kwa kuwapigilia misumari wahalifu, mikono na miguu,

·  Ama kwa kuwafungia kwa kamba mikono na miguu, na kishapo kuusimamisha msalaba na kumwacha mtu afe kwa kushindwa kupumua pale msalabani.

·  Lakini, kwanza kabla ya kusulibishwa msulibiwa alifanyiwa maandalizi ya kumchosha na kumuumiza. Ndipo kwa nia hiyo ya kumwandaa msulibiwa, mhalifu alipigwa kwanza mijeledi.

Pamoja na kumchosha mtu kwa kumpiga mijeledi, mateso mengine aliyopewa mhalifu, yalitegemea ubunifu wa askari wenyewe waliopewa jukumu la kumsulibisha mtu.

·  Ndipo kwa upande wa Yesu, askari watesaji walibuni mbinu za kumvika joho jekundu na kumdhihaki,

·  Wakampiga kwa mwanzi na kumtemea mate.

Awali, Pilato aliwaamuru Yesu atendewe vile, kusudi iwe ndiyo adhabu yake na kishapo aachiliwe huru. Kumbe, baada ya kutendewa hayo na Yesu kurudishwa tena mahakamani, alipowauliza Wayahudi kama walipenda Yesu aachiliwe huru, wao walikataa katakata na badala ya Yesu Wayahudi walichagua Pilato amwachilie huru Baraba. Hapo alishaangushwa katika mradi wake wa kumsamehe Yesu.

Tayari kwa kwenda kusulibiwa, msulibiwa alipaswa kuchukua mwenyewe boriti la kukingama kwa vile boriti la wima lilikuwako tayari kwenye sehemu ya kusulibishia wahalifu. Humo njiani, kama msulibiwa alionesha alama za kuchoka sana kwa kuangukaanguka, askari waliweza kumlazimisha mtu ye yote asaidie kuchukua boriti analoanguka nalo msulibiwa (rej. Mt 27:32).

·  Msulibiwa aliongezewa mateso pamoja na

·  Aibu kwa kusulibiwa hadharani, ambapo kila mtu atamwona na kumtukana au kumfyolea.

· Zaidi ya hayo, alisulibiwa uchi na mbele ya jamaa na ndugu zake.

Nguo za msulibiwa zilikuwa haki ya watesi wake kugawana, kama zilitengana moja moja, zoezi la kugawana lilikuwa rahisi sana, lakini nguo zingine zilipasa kuzipasua na kugawana vipande (rej. Yn 19:23-24).

·  Watesi wa Yesu waligawana vile vile nguo zake baada ya kuziweka katika mafungu manne. Lakini ilipofikia zamu ya kanzu, hawakuweza kugawana kwani haikuwa na mshono, ndipo ilipopigiwa kura ili aitwae askari mmoja tu.

· Kwa hesabu ya mafungu, yaonekana askari waliomsulibisha Yesu walikuwa hasa wanne.

Ilikuwa ni kawaida, askari kubaki pale aliposulibiwa mtu mpaka atakapokufa, isije watu wanaomwonea huruma msulibiwa wakamwokoa na kumtorosha.

Aidha, kwa kumpunguzia maumivu, ilikuwepo kanuni ya kumpa mtu divai iliyochanganywa na dawa ya kumpunguzia maumivu. Lakini, Yesu aliikataa pale alipopewa dawa hiyo (rej. Mt 27:34).

Yote haya, Yesu alifanyiwa na watesi wake kwa ajili yetu sis wanadamu. Yatupasa kukiri kwamba, Bwana wetu aliteseka sana kwa ajili yetu. Tukikumbuka kwa mateso hayo, yalipaswa kwa kweli kila mmoja yamfike binafsi yake, basi hatuna lingine, bali kumiminikwa na shukrani nyingi.

5. YESU ALISULIBIWA MAHALI GANI? IJUMAA KUU

Kwa kadiri ya ukuta wa mji wa Yerusalemu, enzi zile za Yesu, Yesu alisulibiwa nje ya mji, kwenye kilima kidogo cha jiwe kilichoitwa Golgota. Palikuwa mahali pa wazi na watu wengi walikuwa wakipita hapo (rej. Mt 27:39). Ndivyo ilivyopasa kuwa mahali pa kusulibishia watu, kwani watesaji walikusudia kumwaibisha msulibiwa na kumtundika pale kama onyo na kitisho kwa wakorofi wengine.

Ndipo basi, watu wengi walipopatiwa nafasi ya kumtukana na kumfyolea msulibiwa. Adhabu ya kusulibiwa haikuwa adhabu inayotolewa kwa siri hata mara moja. Karibu na Golgota palikuwa na machimbo ya mawe, ambapo watu walikuwa wakichimba mawe kwa ajili ya shughuli za ujenzi mjini. Hata hivyo, kwa pembeni kidogo kulikuwa na bustani. Miamba iliyokuwako hapo ilimpelekea Yusufu wa Arimathea ajichongee kaburi lake pale.

Golgota, enzi zile za Yesu, palikuwa nje ya mji. Lakini kwa kadiri mji ulivyozidi kukua, mahali hapo paliingia ndani ya mji. Leo hii ni karibu katikati ya Yerusalemu ya zamani.

Kanisa moja kubwa limejengwa na kumeza Golgota pamoja na kaburi la Yesu, maana sehemu hizo zilikaribiana (rej. Yn 19:41). Hivi basi, Golgota na kaburi la Yesu viko ndani ya Kanisa moja siku hizi. Mahali linaposimama Kanisa hilo, pametifuliwa na kujengwa mara nyingi.

· Kwanza, Kaisari Hadrian alijenga hekalu la Aphrodite, yaani baada ya uasi wa Wayahudi dhidi ya Warumi mnamo miaka ya 132-135.

· Kaisari Konstantino alilibomoa hekalu hilo akajenga kanisa kubwa, basilika, ambalo lilibomolewa na Waajemi, mnamo mwaka 614, lakini likajengwa upya.

· Kanisa lililopo hapo sasa hivi, lilijengwa na wapiganaji wa Vita vya Msalaba tangu mwaka 1099 na kanisa lenyewe lilitabarukiwa mnamo mwaka 1149.

Jina la mahali aliposulibiwa Yesu lilikuwa Golgota, kutokana na neno la Kiaramayo "gulgulta" yaani "fuvu". Katika Kigiriki, jina hilo lilitafsiriwa kama "kranion". Basi, ndipo mahali hapo pakaitwa kwa Kigiriki "kraniou topos", yaani "mahali pa fuvu". Biblia ya Kilatini cha kawaida, yaani Vulgate ilipotengenezwa, ikatafsiri _"kraniou topos" kama "calvariae locus" na huo ukawa ndio mwanzo wa jina la "Kalvari".

Kwa nini mahali hapo paliitwa "fuvu", hatuna mbinu za kuvumbua ukweli halisi hadi sasa hivi. Lakini kuna pande mbili kuu za maoni,

· Upande mmoja unadai kwamba, kilima chenyewe kilifanana na fuvu la mtu,

· Wakati upande mwingine unadhani kuwa, mahali hapo palikuwa pana mafuvu ya watu waliopata kusulibiwa hapo, lakini wakaachwa bila kuzikwa. Mjadala huu unaendelea hadi hapo ukwei utakapopatikana.

6. AKINA NANI WALIOSHUHUDIA KIFO CHA YESU?

Tukikusanya taarifa kutoka Injili zote nne, tunaona kwamba, kifo cha Yesu kilishuhudiwa na watu wengi sana. Hilo hatuna mashaka nalo.

· Walikuwapo watesi wake, askari ambao hawakupungua wanne, hao ndio waliogawana nguo za Yesu kwa kuzigawa katiki mafungu manne, lakini wakashindwa kuigawa kanzu yaki ambayo haikuwa na mshono wo wote (rej. Yn 19:23-24).

·  Wengine waliokuwapo ni wakuu wa makuhani (rej. Mt 27:41 na
·  Mashabiki au wapambe wao ( rej. Lk 23:35) na

· Wanyang'anyi wawili, mmoja kushoto na mwingine kulia (rej. Yn 19:18).
· Kishapo walikuwapo wanawake waliokuwa akifuatana nao wakati wa kazi yake ya kuutangaza ufalme wa Mungu na
· Jamaa zake,
· Pamoja na mwanafunzi yule aliyempenda. Wanafunzi wengine walikuwa wamelala mbele.

Baadhi ya wanawake waliokuwa pale, walikuwa wakijulikana kwa jina la Maria au Mariamu (rej. Mk 15:40, Yn 19:25). Tunasoma katika Mk 15:40 hivi:

"Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao walikuwamo Mariamu Magdalene na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose na Salome, hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu".

Katika Yn 19: 25 twasoma hivi: "Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Kleopa na Mariamu Magdalene".

Nukuu hizi mbili ni muhimu sana katika kututatulia swali, kama Maria alikuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu. Marko anapomtaja Mariamu mmojawapo kuwa alikuwa mama wa akina Yakobo mdogo na Yose na Salome, bila kusema kwa mkato kuwa alikuwa ndiye mama yake Yesu, tunaelezwa kwamba akina Yakobo, Yose na Salome hawakuwa ndugu wa damu wa Yesu, bali ndugu zake kwa Mariamu aliyekuwa jamaa au dada ya Bikira Maria.

Ndipo basi, inapotupasa kuelewa Mk 6:3 kwamba akina Yakobo, Yose na Yuda na maumbu wao, walikuwa ni ndugu waliokuwa wakiishi katika familia ya akina Yesu kutokana na ujamaa tu. Yaani, hawakuwa watoto wa Bikira Maria.

Maneno "kaka", "ndugu" na "dada" kati ya Wayahudi, hayakumaanisha "ndugu wa damu" tu, bali yalikuwa yakitumika kwa mapana, kwani wao walikuwa na utamaduni wa familia pana, kama ilivyo kati yetu Waafrika.

Tunasema hivi, kutokana na lugha. Mwinjili Yohane anamtaja Bikira Maria kwa mkato akimwita "mamaye" Yesu. Marko kama angelikuwa akimzungumzia Mariamu aliyekuwa mama wa damu wa Yesu asingelimtaja kwa kuwataja watoto wake wengine, bali angelisema moja kwa moja "mamaye" kama alivyomtaja Yohane. Hiyo ndiyo lugha, ina vimilikishi, "yangu", "yake" na kadhalika.

Ushuhuda mwingine kwamba, hao wanaotajwa kuwa ndugu na dada wa Yesu hawakuwa ndugu au dada kwa damu, ni kitendo anachofanya Yesu katika saa hiyo ya kifo. Alimkabidhi mama yake kwa mwanafunzi aliyempenda. Kwa kweli, hii inaonesha jinsi alivyokuwa peke yake. Watoto wa kiyahudi walitazamiwa kuwatunza wazazi wao, kama ilivyotafsirika amri ya nne ya Mungu: "Waheshimu baba na mama yako, siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na BWANA Mungu wako" (Kut 20:12)

Mzazi hawezi kukabidhiwa kwa rafiki, wakati watoto wake wa kuwazaa wangalipo. Tena, tendo hilo linaashiria pia kwamba Yosefu, mume wa Maria, alikuwa ameshafariki. Maana angelikuwapo, wajibu wa kumtunza mkewe ungelikuwa unaendelea tu.

Tumesema mengi ya ziada, sasa hebu turejee kwenye mada ya msingi. Tulikusudia kusema mashahidi wa mateso na kifo cha Yesu walikuwa wengi. Hivyo, kufa kwake kulikuwa kweli na Yesu "hakuwaingiza mjini" watazamaji. Macho yaliyokuwapo yalikuwa ni mengi, kama Yesu angelizimia tu wangelijua na kama angeliwatoroka, wangelijua vile vile.

Fr. Innocent Bahati Mushi OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI).

No comments:

Post a Comment